Monday, August 5, 2013

"Nina msuli wa kuweza kuwasaidia".


Kusanya, kusanya… nakusanya,
Kusanya, kusanya… nakusanya,
Kama magari…nakusanya,
Nyumbanzuri… nakusanya

Hii ni moja kati ya beti za wimbo  wa Anameremeta, wimbo ambao Katapila amezoea kuuimba madhabahuni Ubungo Kibangu, ikiwa pia ni nyimbo moja wapo kati ya zile alizoziimba jana katika ibada ya Jumapili.

Mimi ninawasalimu katika jina la Bwana, yeye aliyeziumba mbingu na nchi.

Kama kawaida kazi yangu ni moja tu katika ukurasa huu, kukujuza kile ambacho kinajiri katika madhabahu ya Ubungo Kibangu, kwa Mzee wa Upako, Antony Lusekelo.

Kwa jumapili ya jana yaani ya tarehe 4/8/2013, ibada ilikuwa ya tofauti kabisa na utaratibu uliyozoeleka, ambapo Mzee wa Upako aliwakaribisha watu mbalimbali kupita madhabahuni na kisha kushuhudia mambo ambayo Mungu ametenda, katika maisha yao.

Kwa hakika shuhuda za wakinamama, waliyojaliwa kupata watoto baada ya maombi kutoka kwa mpakwa mafuta, Mchungaji Antony Lusekelo, zilikuwa lukuki, huku shuhuda nyingine nazo zikiwepo.

Kwa upande wa shuhuda za wale wakinamama waliyo bahatika kupata watoto, zilifunguliwa dimba na mwanamama aliyekaa katika ndoa yake kwa takribani miaka mitano bila mtoto, lakini baada ya maombi sasa anamtoto.

Shuhuda za aina hiyo hazikuishia hapo kwani alikuwepo pia mwanadada aliyekaa katika ndoa yake kwa miaka mitatu bila kupata mtoto, lakini baada tu yatamko la mwaka jana, kutoka kwa Mchungaji Antony Lusekelo kuwa mwakani matasa watazaa, naye kwasasa amebahatika kupata watoto mapacha wawili, tena wote wakiwa ni wanaume.

Hatimaye shuhuda za kupata watoto zilifungwa na mwanamama aliyekaa kwa miaka kumi na mitano bila ya kupata mtoto mwingine ambapo alikuwa na mtoto wa kiume pekee (15), lakini baada ya maombi kutoka kwa Katapila, na yeye amebahatika kupata mtoto wa pili.

Kwa amahakika shuhuda hizo ziliwagusa sana watu wote waliokuwepo kanisani hapo jana, lakini huo haukuwa mwisho washuhuda kwani walipita pia watu wengine wengi kushuhudia mambo ambayo Mungu Baba amewatendea kupitia madhabahu ile yaUbungo, Kibangu.

Shuhuda hizo ni kama zile za kazi, magari, viwanja, na mafanikio ya aina tofautitofauti ndizo ambazo zilitawala katika madhabahu ile kwa siku ya jana, jambo lililomfanya kila muumini aliyefika kanisani hapo kwa siku ya jana, abaki kulitukuza na kulishangaa jina la Yesu, kupitia mkono wa Mtumishi wake.

Kwa ufupi hivi ndivyo ilivyokuwa jana, kwa Transformer, lakini nje ya hapo ibada ilitawaliwa sana na nyimbo mbalimbali zilizokuwa zikiimbishwa na Mchungaji mwenyewe, huku maombi yakitosha pia yakiwepo.

hata hivyo baada ya yote hayo, Mzee wa Upako, hakusita kuwahakikishia  watu wote kuwa ni lazima mwaka huu kieleweke katika mipango na mahitaji ya kila mmoja.

“Nina msuli wa kuweza kuwasaidia ninyi nyote, na wala sioni haya kusema haya, kwani nina Supa chaji kutoka kwa baba” aliongeza Mzee wa Upako, Mchungaji Antony Lusekelo.

Mimi nikutakie wiki njema, yenye mafanikio tele pamoja na baraka mpaka pale tutapokutana tena hapa siku ya Ijumaa, ambapo nitakuhabarisha kile kilichojiri Alhamisi GRC Ubungo, Kibangu.

Barikiwa!


0 comments:

Post a Comment