Friday, August 2, 2013

OMBA PASIPO KUKATA TAMAA.


Watashindanaaaaa!
Natumai umzima na upo tayari kujua kile ambacho kilijiri madhabahuni mwa bwana, Ubungo Kibangu kwa Mzee wa Upako, jana Alhamisi ya tarehe 1/8/2013. 

Kwa wale wenzangu na mie tuliyoweza kufika madhabahuni hapo, naamini kabisa tulipata kitu cha tofauti ndani ya mioyo yetu, tangu pale tulipoanza kwa kumsifu Mungu na kumwabudu (Praise & Worship), mpaka alipoingia baba yetu wa kiroho, Mchungaji Antony Lusekelo.

Kama kawaida tuliabudu kwa pamoja na baada ya hapo, Mzee wa Upako aliongoza sala iliyojaa utulivu wa roho mtakatifu, huku akimwomba Mungu atuonekanie tangu kwenye ibada ile, hata katika maisha yetu kwa ujumla.  

Baada ya maombi hayo, tulimsifu Mungu huku tukiongozwa na yeye (Mchungaji), kwa pambio la ‘Yesu namba moja’ ambapo kwa hakika tulilitukuza jina la Bwana Yesu kwa furaha kuu, na kisha tukaingia katika neno.


Ujumbe: OMBA PASIPO KUKATA TAMAA.
Neno; Luka 18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.
Hili ndilo somo, pamoja na neno lililotumika hiyo jana, yaani Alhamisi ya tarehe mosi, mwezi wa nane.

Mchungaji alianza kulielezea neno hili, kwa kutoa mfano kuwa wapo watu wengi ambao hulalamika sana kwamba, wameombewa katika makanisa mengi pasipo mafanikio, na kusema kuwa wengi wao hukata tamaa njiani huku wengine wakitaka kumtumia Mungu kama njia tu ya kutokea, na si kwamba wanampenda na kumuhitaji. 

“Mara nyingi tunashindwa kufanikiwa, kwasababu hatumtaki Mungu, tunataka nguvu zake tu” alisema Katapila na kuongeza kuwa, kwa mtindo huo kamwe hatuwezi kumwona Yawe.

Katika kusisitiza hilo, Mchungaji alisema kuwa inampasa kila mtu kumwamini Mungu na kumpenda, na si kuishia kuzipenda kazi zake tu, kwa mfano wa baadhi ya watu waliyomfuata Yesu kwasababu ya mikate.

Vilevile Mchungaji aliwekawazi kwamba katika maombi yoyote yale, ni lazima msingi mkuu wa maombi hayo uwe ni bidii pamoja na imani, itakayokufanya wewe usikate tamaa.

Kukata tamaa ni jambo ambalo Mchungaji alilikemea kwa nguvu na mifano mbalimbali, kama ule wa Mitume kumi na wawili ambapo baada ya kupaa kwa Yesu, wanafunzi hao walipitia magumu mengi ikiwemo kuuawa kwa Yakobo (mwanafunzi wa Yesu).

“Jambo hili la kuuawa kwa Yakobo halikuwakatisha tamaa wanafunzi wa Yesu, wala halikuwafanya wakufuru, zaidi tu walizidi kusongambele na hatimaye wakaweza kuijenga misingi imara ya Kanisa” alisema Transformer.

Ni wazi kuwa mtumishi huyu wa Mungu, alikuwa akijenga roho ya kumtumaini bwana mioyoni mwetu,pamoja na roho ya bidii katika kumlilia Mungu kwenye mahitaji yetu, vitu ambavyo tunaweza kuvitumia kama nyenzo ya kufika kule tuendako.

Lakini kutokana na ukaribu aliyonao Mchungaji Lusekelo kwa Mungu, na katika kuzidi kufafanua zaidi juu ya maombi, yeye aliweka wazi jambo fulani na kusema kuwa, ”Ukiombewa na mimi halafu usifanikiwe, nenda uendako hutofanikiwa wala kupona milele, kwasababu najua Mungu anavyonisikia”.

Kauli hii inaonyesha wazi kuwa, kumbe nae mtumishi huyu wa Mungu huomba kwa bidii, na kwa dhati kiasi cha kuamini kuwa kama hitaji lako lisipoisha ukiwa katika madhabahu ile ya Ubungo Kibangu, basi hitaji hilo halitoweza kuisha mahali popote pale, chini ya jua. 

Ni wazi kuwa maombi yana nguvu na huwatoa watu katika vifungo mbalimbali vya magonjwa, laana, mikosi, umasikini na kila hila za Yule muovu shetani na ndiyo maana Mchungaji Antony Lusekelo, kwa siku ya Alhamisi ya jana, aliamua kusisitizia suala la kuomba pasipo kuchoka wala kukata tamaa, mpaka pale Mungu atakapo jibu mahitaji yetu.

Kwa kifupi hayo ndiyo yaliyojiri jana katika madhabahu ya Ubungo Kibangu, kwa Mzee wa Upako.  

Karibu nawe Jumapili ya tarehe 4/8/2013, tuabudu pamoja na kujifunza mengi juu ya Ufalme wa Mungu aliyetuumba. 

Jinsi ya kufika; Panda gari la Ubungo, shuka Riverside kituo ambacho kipo karibu na LandMark Hoteli, hapo utaona bango la Mtumishi wa Mungu Antony Lusekelo, linaloelekeza njia ya kuelekea kanisani. Waweza panda pikipiki, taxi au mabasi ya kanisa yanayosafirisha waumini, BURE!

Kwa mawasiliano ya ujumbe mfupi wa maandishi (sms); +255(0)713 725 473.

Watashindana, lakini hawatashinda!
Tutapanga mipango, itapangika!
Wakituloga, imekula kwao!
Kwetu, hakuna kudumaa!  

0 comments:

Post a Comment