Shalom! Shalom!
Watashindanaaa! Lakini hawatashinda.
Hizi ni baadhi tu ya salamu tunazoweza salimiana sisi
tumwaminio Kristo Yesu, na tuliyo katika madhabahu ya Bwana inayoongozwa na
Mchungaji, Antony Lusekelo (supa chaji).
Nikukaribishe basi katika safu hii, ambapo kama kawaida
unapata nafasi ya kujua kile kilichojiri katika madhabahu ya Ubungo, Kibangu
katika siku zote za Ibada.
Ndani ya juma hili ambalo lilikuwa na wingi wa sherehe
za kitaifa kwa maana ya nane nane, pamoja na sherehe ile ya kidini ya ndugu
zetu Waislamu (Eid Mubarak), Mchungaji Antony Lusekelo alikuwa na mfululizo wa
somo alilolipa jina la Mambo ya sirini,
aliyonayo mwanadamu.
Somo hili lilianza rasmi katika siku ya Alhamisi, huku
Mchungaji akiviweka bayana vitu hivyo vya sirini alivyonavyo binadamu, kuwa ni roho, malaika, pamoja na nyota, ambapo
kwasasa alizama katika elimu ya nyota.
Ni wazi kuwa kwa kipindi sasa Wakristo tumeyatupilia
mbali masomo ya nyota, tukiamini kuwa huwenda imani hiyo iko nje ya imani
tuliyonayo, suala ambalo Mchungaji anaweka wazi kuwa si sahihi.
Katika ibada ya juzi, yaani ya Jumapili ya tarehe 11
mwezi agosti, Katapila aliamua kuutoa utata huo kwa kusema kuwa, kila
binadamu anayo nyota yake, nyota ambayo inamtofautisha na mtu mwingine yeyote.
Aidha Mchungaji alitoa mfano wa Yusufu alipokuwa
akiwaelezea familia yake juu ya ndoto yake, aliyoota nyota zikimwatamia pamoja
na mfano wa Mamajusi wa Mashariki, waliyoiona nyota ya Kifalme ya Kristo Yesu Mnazareti,
kama udhihirisho tu wa kuwa kila mtu anayo nyota yake.
Katika kudadavua zaidi somo hili la nyota kupitia
Biblia, huku akiweka wazi kuwa nyota yaweza kufishwa au kung’azwa, Katapila
alisoma neno;
Neno: Ufununo wa Yohana 2:26-28.
“26Na
yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya
mataifa.27naye
atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama
mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.28Nami
nitampa ile nyota ya asubuhi.”
Mchungaji alisema kuwa nyota ya mtu ndiyo inayoweza
kumsababishia kibali kwa watu, baraka, mafanikio, na hata maendeleo. Ila endapo nyota hiyo itafishwa, ndipo
ambapo mikosi, laana, ajali, kudidimia kimaisha
na mambo mengine mabaya kama hayo, humpata mtu.
“mtaa unaokaa, pamoja na watu unaokaa nao wanaweza
kufisha nyota yako, na ndiyo maana
nitakuombea asubuhi ya leo juu ya nyota hiyo, Mungu airudishe na ing’ae”
aliongeza Mchungaji.
Mengi aliyasema King Kong katika suala hili la nyota,
lakini haswahaswa alikuwa akisisitiza kuwa, inampasa kila mtu kumwomba Mungu
juu ya nyota yake, kwani ni moja kati ya vitu vya muhimu katika maisha ya
mwanadamu.
Hata hivyo Mchungaji hakuishi hapo, kwani aliwaonya
watu juu ya uadui na kusema kuwa, si vyema mtu akatengeneza maadui huku
akikataza pia watu kuuwana pasipo sababu.
Dokezo.
(Haya ni baadhi tu ya maneno aliyoyasema, na kuyahubiri Mchungaji Lusekelo Antony,
akisindikizia somo la siku).
“ukija kanisani, shiriki kila jambo, na acha kudandia
treni kwa mbele”.
“mimi ni Mchungaji niliyosomea sana wito wangu, na nina
uzoefu wa miaka zaidi ya 30”.
“elimu ni zaidi ya kukaa darasani,. Elimu ni uwezo wa
kuyatawala mazingira yako”.
“kama wewe ni kijana, soma sana katika fani yako, kwani
Biblia imesema Mshike sana elimu, usimuache aende zake”.
“wamebarikiwa sana wanaomjua bwana Mungu wao. Mjue sana
Mungu, ndipo mema yatakavyo kuijilia”.
“ibada hizi zinakusogeza karibu na Mungu. Pia
itakurudishia kiu ya kwenda, kanisani”.
“upandacho, ndicho utakachovuna. Usimtende ubaya mtu
anayekuamini”
“usishindane na asiyekudhuru, wala kupanga kumpiga mwenzako,
kwa siri ni mwiko”.
“unapompa mtu nafasi ya kukujua, unampa shetani nafasi.
Mfano ni Samsoni, alimpa nafasi Delila ya kumjua”.
“mwanamke au mwanaume, anapokuja au mnapokutana na
rafiki wa mumeo au mkeo, acha kuchangamka sana, mkaribishe kisha kaa mbali
waache waongee kama wanaume kwa wanaume, au wanawake kwa wanawake na si
kuyatawala maongezi yao”.
“mwiko kuitawala nyumbaya mwanaume mwenzio, wala
kumuita mwanaume mwenzio bwana mdogo mbele ya mkewe, hata kama umemzidi umri”.
“Muheshimu mtu kwa wajibu wake”.
“Ukimkuta kijana anaumri wa miaka arobaini na ana
nyumba 3, halafu wewe huna japo umemzidi umri, ni Mzee kwako, muheshimu na umpe
shikamoo!”
Kwa mengi au kwa machache, hayo ndiyo yaliyojiri
Jumapili ya jana madhabahuni kwa bwana GRC, Ubungo Kibangu kwa Mchungaji
Lusekelo Antony maarufu kama Katapila, au Mzee wa Upako.
Uwe na wiki njema.
Barikiwa!






0 comments:
Post a Comment