Mwanzo 1:20

Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu.

Mwanzo 1:12

Nchi ikaota majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake,na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.

Zaburi 24:1-2

Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake. Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari, Na juu ya mti ya maji aliithibitisha.

Yoeli 2:1

Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu; Wenyeji wote wa nchi na watetemeke; Kwa maana siku ya Bwana inakuja. Kwa sababu inakaribia.

Yeremia 1:18-19

Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo za chuma, na kuta za shaba; juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe.

Thursday, August 29, 2013

Askofu Moses Kulola amefariki dunia.

Marehemu Askofu Kulola akihubiri.

Taarifa ambazo zimetufikia hivi punde zinasema kuwa Askofu Mkuu wa Evangelistic Assemblies God Tanzania, Moses Kulola amefariki dunia takriban dakika 25 zilizopita.

Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika ambazo mtandao huu imezipata kutoka kwa watu wa ndani wa familia hiyo, zinaeleza kuwa Askofu Kulola amefariki katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam.

Askofu Kulola, ambaye amezaliwa mwaka 1928, amekuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu na hata kufikia hatua ya kupelekwa nchini India kwa matibabu.

Katika uhai wake, amepata watoto wengi wa kiroho ikiwemo Dr Daniel Kulola, Mchungaji Florian Katunzi, Zakaria Kakobe, Maboya, Mwasota na wengineo wengi.


Blogi hii itaendelea kukufahamisha kwa kadri ambavyo taarifa zitakuwa zikitufikia.Kufahamu historia ya maisha ya Hayati Askofu Dr. Moses Kulola

BWANA ametoa na BWANA ametwaa, jina la BWANA lihimidiwe.

Tuesday, August 13, 2013

Mambo ya sirini aliyonayo mwanadamu.


Shalom! Shalom!

Watashindanaaa! Lakini hawatashinda.

Hizi ni baadhi tu ya salamu tunazoweza salimiana sisi tumwaminio Kristo Yesu, na tuliyo katika madhabahu ya Bwana inayoongozwa na Mchungaji, Antony Lusekelo (supa chaji).

Nikukaribishe basi katika safu hii, ambapo kama kawaida unapata nafasi ya kujua kile kilichojiri katika madhabahu ya Ubungo, Kibangu katika siku zote za Ibada.

Ndani ya juma hili ambalo lilikuwa na wingi wa sherehe za kitaifa kwa maana ya nane nane, pamoja na sherehe ile ya kidini ya ndugu zetu Waislamu (Eid Mubarak), Mchungaji Antony Lusekelo alikuwa na mfululizo wa somo alilolipa jina la Mambo ya sirini, aliyonayo mwanadamu.

Somo hili lilianza rasmi katika siku ya Alhamisi, huku Mchungaji akiviweka bayana vitu hivyo vya sirini alivyonavyo binadamu, kuwa ni roho, malaika, pamoja na nyota, ambapo kwasasa alizama katika elimu ya nyota.

Ni wazi kuwa kwa kipindi sasa Wakristo tumeyatupilia mbali masomo ya nyota, tukiamini kuwa huwenda imani hiyo iko nje ya imani tuliyonayo, suala ambalo Mchungaji anaweka wazi kuwa si sahihi.

Katika ibada ya juzi, yaani ya Jumapili ya tarehe 11 mwezi agosti, Katapila aliamua kuutoa utata huo kwa kusema kuwa, kila binadamu anayo nyota yake, nyota ambayo inamtofautisha na mtu mwingine yeyote.

Aidha Mchungaji alitoa mfano wa Yusufu alipokuwa akiwaelezea familia yake juu ya ndoto yake, aliyoota nyota zikimwatamia pamoja na mfano wa Mamajusi wa Mashariki, waliyoiona nyota ya Kifalme ya Kristo Yesu Mnazareti, kama udhihirisho tu wa kuwa kila mtu anayo nyota yake.

Katika kudadavua zaidi somo hili la nyota kupitia Biblia, huku akiweka wazi kuwa nyota yaweza kufishwa au kung’azwa, Katapila alisoma neno;

Neno: Ufununo wa Yohana 2:26-28. 

26Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa.27naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.28Nami nitampa ile nyota ya asubuhi.

Mchungaji alisema kuwa nyota ya mtu ndiyo inayoweza kumsababishia kibali kwa watu, baraka, mafanikio, na hata  maendeleo. Ila endapo nyota hiyo itafishwa, ndipo ambapo mikosi, laana, ajali, kudidimia kimaisha  na mambo mengine mabaya kama hayo, humpata mtu.

“mtaa unaokaa, pamoja na watu unaokaa nao wanaweza kufisha nyota yako,  na ndiyo maana nitakuombea asubuhi ya leo juu ya nyota hiyo, Mungu airudishe na ing’ae” aliongeza Mchungaji.

Mengi aliyasema King Kong katika suala hili la nyota, lakini haswahaswa alikuwa akisisitiza kuwa, inampasa kila mtu kumwomba Mungu juu ya nyota yake, kwani ni moja kati ya vitu vya muhimu katika maisha ya mwanadamu.

Hata hivyo Mchungaji hakuishi hapo, kwani aliwaonya watu juu ya uadui na kusema kuwa, si vyema mtu akatengeneza maadui huku akikataza pia watu kuuwana pasipo sababu.

Dokezo.
(Haya ni baadhi tu ya maneno aliyoyasema, na kuyahubiri Mchungaji Lusekelo Antony, akisindikizia somo la siku).

“ukija kanisani, shiriki kila jambo, na acha kudandia treni kwa mbele”.

“mimi ni Mchungaji niliyosomea sana wito wangu, na nina uzoefu wa miaka zaidi ya 30”.

“elimu ni zaidi ya kukaa darasani,. Elimu ni uwezo wa kuyatawala mazingira yako”.

“kama wewe ni kijana, soma sana katika fani yako, kwani Biblia imesema Mshike sana elimu, usimuache aende zake”.

“wamebarikiwa sana wanaomjua bwana Mungu wao. Mjue sana Mungu, ndipo mema yatakavyo kuijilia”.

“ibada hizi zinakusogeza karibu na Mungu. Pia itakurudishia kiu ya kwenda, kanisani”.

“upandacho, ndicho utakachovuna. Usimtende ubaya mtu anayekuamini”
“usishindane na asiyekudhuru, wala kupanga kumpiga mwenzako, kwa siri ni mwiko”.

“unapompa mtu nafasi ya kukujua, unampa shetani nafasi. Mfano ni Samsoni, alimpa nafasi Delila ya kumjua”.

“mwanamke au mwanaume, anapokuja au mnapokutana na rafiki wa mumeo au mkeo, acha kuchangamka sana, mkaribishe kisha kaa mbali waache waongee kama wanaume kwa wanaume, au wanawake kwa wanawake na si kuyatawala maongezi yao”.

“mwiko kuitawala nyumbaya mwanaume mwenzio, wala kumuita mwanaume mwenzio bwana mdogo mbele ya mkewe, hata kama umemzidi umri”.

“Muheshimu mtu kwa wajibu wake”.

“Ukimkuta kijana anaumri wa miaka arobaini na ana nyumba 3, halafu wewe huna japo umemzidi umri, ni Mzee kwako, muheshimu na umpe shikamoo!”

Kwa mengi au kwa machache, hayo ndiyo yaliyojiri Jumapili ya jana madhabahuni kwa bwana GRC, Ubungo Kibangu kwa Mchungaji Lusekelo Antony maarufu kama Katapila, au Mzee wa Upako.

Uwe na wiki njema. 

Barikiwa!



Monday, August 5, 2013

"Nina msuli wa kuweza kuwasaidia".


Kusanya, kusanya… nakusanya,
Kusanya, kusanya… nakusanya,
Kama magari…nakusanya,
Nyumbanzuri… nakusanya

Hii ni moja kati ya beti za wimbo  wa Anameremeta, wimbo ambao Katapila amezoea kuuimba madhabahuni Ubungo Kibangu, ikiwa pia ni nyimbo moja wapo kati ya zile alizoziimba jana katika ibada ya Jumapili.

Mimi ninawasalimu katika jina la Bwana, yeye aliyeziumba mbingu na nchi.

Kama kawaida kazi yangu ni moja tu katika ukurasa huu, kukujuza kile ambacho kinajiri katika madhabahu ya Ubungo Kibangu, kwa Mzee wa Upako, Antony Lusekelo.

Kwa jumapili ya jana yaani ya tarehe 4/8/2013, ibada ilikuwa ya tofauti kabisa na utaratibu uliyozoeleka, ambapo Mzee wa Upako aliwakaribisha watu mbalimbali kupita madhabahuni na kisha kushuhudia mambo ambayo Mungu ametenda, katika maisha yao.

Kwa hakika shuhuda za wakinamama, waliyojaliwa kupata watoto baada ya maombi kutoka kwa mpakwa mafuta, Mchungaji Antony Lusekelo, zilikuwa lukuki, huku shuhuda nyingine nazo zikiwepo.

Kwa upande wa shuhuda za wale wakinamama waliyo bahatika kupata watoto, zilifunguliwa dimba na mwanamama aliyekaa katika ndoa yake kwa takribani miaka mitano bila mtoto, lakini baada ya maombi sasa anamtoto.

Shuhuda za aina hiyo hazikuishia hapo kwani alikuwepo pia mwanadada aliyekaa katika ndoa yake kwa miaka mitatu bila kupata mtoto, lakini baada tu yatamko la mwaka jana, kutoka kwa Mchungaji Antony Lusekelo kuwa mwakani matasa watazaa, naye kwasasa amebahatika kupata watoto mapacha wawili, tena wote wakiwa ni wanaume.

Hatimaye shuhuda za kupata watoto zilifungwa na mwanamama aliyekaa kwa miaka kumi na mitano bila ya kupata mtoto mwingine ambapo alikuwa na mtoto wa kiume pekee (15), lakini baada ya maombi kutoka kwa Katapila, na yeye amebahatika kupata mtoto wa pili.

Kwa amahakika shuhuda hizo ziliwagusa sana watu wote waliokuwepo kanisani hapo jana, lakini huo haukuwa mwisho washuhuda kwani walipita pia watu wengine wengi kushuhudia mambo ambayo Mungu Baba amewatendea kupitia madhabahu ile yaUbungo, Kibangu.

Shuhuda hizo ni kama zile za kazi, magari, viwanja, na mafanikio ya aina tofautitofauti ndizo ambazo zilitawala katika madhabahu ile kwa siku ya jana, jambo lililomfanya kila muumini aliyefika kanisani hapo kwa siku ya jana, abaki kulitukuza na kulishangaa jina la Yesu, kupitia mkono wa Mtumishi wake.

Kwa ufupi hivi ndivyo ilivyokuwa jana, kwa Transformer, lakini nje ya hapo ibada ilitawaliwa sana na nyimbo mbalimbali zilizokuwa zikiimbishwa na Mchungaji mwenyewe, huku maombi yakitosha pia yakiwepo.

hata hivyo baada ya yote hayo, Mzee wa Upako, hakusita kuwahakikishia  watu wote kuwa ni lazima mwaka huu kieleweke katika mipango na mahitaji ya kila mmoja.

“Nina msuli wa kuweza kuwasaidia ninyi nyote, na wala sioni haya kusema haya, kwani nina Supa chaji kutoka kwa baba” aliongeza Mzee wa Upako, Mchungaji Antony Lusekelo.

Mimi nikutakie wiki njema, yenye mafanikio tele pamoja na baraka mpaka pale tutapokutana tena hapa siku ya Ijumaa, ambapo nitakuhabarisha kile kilichojiri Alhamisi GRC Ubungo, Kibangu.

Barikiwa!


Friday, August 2, 2013

OMBA PASIPO KUKATA TAMAA.


Watashindanaaaaa!
Natumai umzima na upo tayari kujua kile ambacho kilijiri madhabahuni mwa bwana, Ubungo Kibangu kwa Mzee wa Upako, jana Alhamisi ya tarehe 1/8/2013. 

Kwa wale wenzangu na mie tuliyoweza kufika madhabahuni hapo, naamini kabisa tulipata kitu cha tofauti ndani ya mioyo yetu, tangu pale tulipoanza kwa kumsifu Mungu na kumwabudu (Praise & Worship), mpaka alipoingia baba yetu wa kiroho, Mchungaji Antony Lusekelo.

Kama kawaida tuliabudu kwa pamoja na baada ya hapo, Mzee wa Upako aliongoza sala iliyojaa utulivu wa roho mtakatifu, huku akimwomba Mungu atuonekanie tangu kwenye ibada ile, hata katika maisha yetu kwa ujumla.  

Baada ya maombi hayo, tulimsifu Mungu huku tukiongozwa na yeye (Mchungaji), kwa pambio la ‘Yesu namba moja’ ambapo kwa hakika tulilitukuza jina la Bwana Yesu kwa furaha kuu, na kisha tukaingia katika neno.


Ujumbe: OMBA PASIPO KUKATA TAMAA.
Neno; Luka 18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.
Hili ndilo somo, pamoja na neno lililotumika hiyo jana, yaani Alhamisi ya tarehe mosi, mwezi wa nane.

Mchungaji alianza kulielezea neno hili, kwa kutoa mfano kuwa wapo watu wengi ambao hulalamika sana kwamba, wameombewa katika makanisa mengi pasipo mafanikio, na kusema kuwa wengi wao hukata tamaa njiani huku wengine wakitaka kumtumia Mungu kama njia tu ya kutokea, na si kwamba wanampenda na kumuhitaji. 

“Mara nyingi tunashindwa kufanikiwa, kwasababu hatumtaki Mungu, tunataka nguvu zake tu” alisema Katapila na kuongeza kuwa, kwa mtindo huo kamwe hatuwezi kumwona Yawe.

Katika kusisitiza hilo, Mchungaji alisema kuwa inampasa kila mtu kumwamini Mungu na kumpenda, na si kuishia kuzipenda kazi zake tu, kwa mfano wa baadhi ya watu waliyomfuata Yesu kwasababu ya mikate.

Vilevile Mchungaji aliwekawazi kwamba katika maombi yoyote yale, ni lazima msingi mkuu wa maombi hayo uwe ni bidii pamoja na imani, itakayokufanya wewe usikate tamaa.

Kukata tamaa ni jambo ambalo Mchungaji alilikemea kwa nguvu na mifano mbalimbali, kama ule wa Mitume kumi na wawili ambapo baada ya kupaa kwa Yesu, wanafunzi hao walipitia magumu mengi ikiwemo kuuawa kwa Yakobo (mwanafunzi wa Yesu).

“Jambo hili la kuuawa kwa Yakobo halikuwakatisha tamaa wanafunzi wa Yesu, wala halikuwafanya wakufuru, zaidi tu walizidi kusongambele na hatimaye wakaweza kuijenga misingi imara ya Kanisa” alisema Transformer.

Ni wazi kuwa mtumishi huyu wa Mungu, alikuwa akijenga roho ya kumtumaini bwana mioyoni mwetu,pamoja na roho ya bidii katika kumlilia Mungu kwenye mahitaji yetu, vitu ambavyo tunaweza kuvitumia kama nyenzo ya kufika kule tuendako.

Lakini kutokana na ukaribu aliyonao Mchungaji Lusekelo kwa Mungu, na katika kuzidi kufafanua zaidi juu ya maombi, yeye aliweka wazi jambo fulani na kusema kuwa, ”Ukiombewa na mimi halafu usifanikiwe, nenda uendako hutofanikiwa wala kupona milele, kwasababu najua Mungu anavyonisikia”.

Kauli hii inaonyesha wazi kuwa, kumbe nae mtumishi huyu wa Mungu huomba kwa bidii, na kwa dhati kiasi cha kuamini kuwa kama hitaji lako lisipoisha ukiwa katika madhabahu ile ya Ubungo Kibangu, basi hitaji hilo halitoweza kuisha mahali popote pale, chini ya jua. 

Ni wazi kuwa maombi yana nguvu na huwatoa watu katika vifungo mbalimbali vya magonjwa, laana, mikosi, umasikini na kila hila za Yule muovu shetani na ndiyo maana Mchungaji Antony Lusekelo, kwa siku ya Alhamisi ya jana, aliamua kusisitizia suala la kuomba pasipo kuchoka wala kukata tamaa, mpaka pale Mungu atakapo jibu mahitaji yetu.

Kwa kifupi hayo ndiyo yaliyojiri jana katika madhabahu ya Ubungo Kibangu, kwa Mzee wa Upako.  

Karibu nawe Jumapili ya tarehe 4/8/2013, tuabudu pamoja na kujifunza mengi juu ya Ufalme wa Mungu aliyetuumba. 

Jinsi ya kufika; Panda gari la Ubungo, shuka Riverside kituo ambacho kipo karibu na LandMark Hoteli, hapo utaona bango la Mtumishi wa Mungu Antony Lusekelo, linaloelekeza njia ya kuelekea kanisani. Waweza panda pikipiki, taxi au mabasi ya kanisa yanayosafirisha waumini, BURE!

Kwa mawasiliano ya ujumbe mfupi wa maandishi (sms); +255(0)713 725 473.

Watashindana, lakini hawatashinda!
Tutapanga mipango, itapangika!
Wakituloga, imekula kwao!
Kwetu, hakuna kudumaa!  

Thursday, August 1, 2013

Mjue vyema Nguli huyu wa Injili hapa nchini.

Mzee wa upako

Anajulikana kwa jina la Mzee wa Upako, Katapila, Transformer, pamoja na majina mengi ambayo amekuwa akipatiwa na waumini wake kutokana tu na nguvu alizonazo za maombi (upako), zinazowafungua watu wengi katika matatizo mbalimbali. Yeye ni baba wa watoto wanne ambao ni Modekai, Salome, Mishaeli, pamoja na Elishadai.  Mkewe ni Bi.Happiness Ngasala, moja kati wa wafanyakazi wa TBC Taifa, huku wote wakiwa ni Wanyakyusa.
Katapila yeye ni mcheshi, mkali kiasi, mkweli, si mnafiki, jasiri katika yale anayoyaamini, pamoja na muwazi huku akiwa na mapenzi ya kweli kwa kila ampendaye na mwenye kuiamini Injili yake.
Katika mahubiri yake, mara zote huyachambua katika hali ya uhalisia huku akionyesha wazi kukerwa na umasikini tuliyonao Watanzania pamoja na Waafrika kwa ujumla.
"Watashindana lakini hawatashinda, tutapanga mipango, itapangika, wakituloga imekula kwao na kwetu hakuna kudumaa", ni baadhi tu ya misemo ya Biblia, inayomtambulisha vyema Mchungaji huyu.